Quantcast
Channel: GABRIEL KILAMLYA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 2276

USIMAMIZI WA FEDHA KATIKA LGAs WABORESHWA

$
0
0




 
 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Hawa Ghasia (Mb), amesema ifikapo mwaka 2015, Halmashauri zote nchini zitakuwa zimeshafanikiwa kuwa na mfumo thabiti wa kuthibiti fedha zote katika Halmashauri zake. Mhe. Ghasia aliyasema hayo akiwa anazungumza na Umma kupitia Vyombo vya habari katika Ukumbi wa Habari – Maelezo.
 
Akizungumza na Waandishi wa Habari, sawa sawa na mzunguko /ratiba iliyoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni, Idara ya Habari – Maelezo, Mhe. Ghasia alijikita katika kuzungumzia usimamizi na udhibiti wa fedha katika Serikali za Mitaa.
 
 
PICHA: Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Hawa Ghasia (Mb.) akizungumza na Umma (Vyombo vya Habari) Kuhusu; Usimamizi wa fedha na udhibiti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, katika Ukumbi wa Habari – Maelezo
 
Pamoja na mambo mengine Mhe. Ghasia alielezea Mikakati mbalimbali inayochukuliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI ili kuhakikisha utendaji mzuri wa kazi unaendelea. Alisema; “ Mbali na kazi inayofanywa na wakaguzi wa ndani, nimewaagiza Manaibu Waziri wa ofisi yangu, kuwa wanapofanya ziara wahakikishe wanafanya ukaguzi kwa kufuatilia matumizi ya fedha na kuhakikisha wanafanya vikao na madiwani na watumishi wa Halmashauri husika”.
 
Maelezo ya Mh. Waziri kwa vyombo vya habari kuhusu usimamizi na udhibiti wa fedha katika mamlaka za serikali za mitaa.
 

 
PICHA: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Hawa Ghasia (Mb.) akizungumza na Umma (Vyombo vya Habari) Kuhusu; Usimamizi wa fedha na udhibiti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, katika Ukumbi wa Habari – Maelezo. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi- Idara ya Serikali za Mitaa/DLG (OWM-TAMISEMI), Bw. Agustino Kalinga na kulia kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari – Maelezo, Bw. Assah Mwambene.
 
Akizungumza kuhusu Halmashauri zinazofanya vizuri; Mhe. Ghasia aliitaja Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kufanya kazi nzuri katika Usimamizi na Ukusanyaji wa Mapato yake, alieleza kuwa moja ya sababu ya Halmashauri ya wilaya ya Temeke kufanikiwa zaidi katika eneo hili ni kutokana na matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki unaotumiwa na Halmashauri hiyo. Aidha alieleza kuwa Halmashauri zote nchini zinatakiwa kuendelea kutumia mfumo huo. Alisema pia Jiji la Mwanza na Mbeya limeonekana kufanya vyema pia katika matumizi ya Mfumo husika. Alitaja pia baadhi ya maeneo mengine yanayofanya kazi nzuri katika eneo hilo kuwa ni pamoja na; Mbinga, Tandahimba na Misungwi. Vile vile Mhe. Ghasia alitaja jiji la Arusha kuonekana kutofanya vyema awali, lakini sasa linaendelea vyema.
 
Aidha pamoja na kuimarika kwa usimamizi wa rasilimali za MSM, kumekuwepo na vitendo vya baadhi ya Watendaji katika ngazi hizo kufuja mali za umma kinyume na taratibu zilizopo. Hata hivyo Serikali imeendelea kuwachukulia Watumishi hao hatua za Kinidhamu na Kisheria kulingana na makosa waliyofanya. Hatua hizi ni pamoja na kufukuzwa kazi, kupewa onyo, kuvuliwa madaraka, kushushwa mshahara, kufikishwa Mahakamani pamoja na kutakiwa kurejesha fedha zilizopotea. Hatua hizo zimekuwa zikichukuliwa pale inapobainika au kuthibitika Watumishi wameshindwa kutekeleza wajibu wao. Hadi kufikia mwezi Septemba, 2013 hatua za Kinidhamu/Kisheria zimechukuliwa kwa Watumishi mbalimbali waliofanya ubadhirifu. Jumla ya Wakurugenzi 53, Wakuu wa Idara 65 na Watumishi wengine 749 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wamechukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu kufuatia kuhusishwa na ubadhirifu wa fedha za umma.
 
Kwa habari zaidi kuhusu maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI); Maelezo ya Taarifa nzima kuhusu Usimamizi na udhibiti wa Fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa imeambatanishwa.
 
 



Viewing all articles
Browse latest Browse all 2276

Trending Articles