Quantcast
Channel: GABRIEL KILAMLYA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 2276

RIPOTI YA KUUNGUA KWA VIAZI MVIRINGO NJOMBE HADHARANI

$
0
0

TAARIFA YA UCHUNGUZI WA UGONJWA WA UKUNGU WA VIAZI MVIRINGO MKOA WA NJOMBE

Afisa Kilimo Mwandamizi Halmashauri ya Mji wa Njombe Nolasco Kilumile Akizungumza na www.gabrielkilamlya.blogspot.com juu ya ripoti ya kuungua kwa viazi.

 UTANGULIZI

Tarehe 18/02/2016 kituo kilipokea taarifa ya mlipuko wa ugonjwa wa kukauka viazi mviringo kutoka mkoa wa Njombe ukiomba tusaidie kubaini tatizo na kushauri jinsi ya kunusuru hali iliyotokea. Tarehe 9/03/2016, timu ya watafiti watano wakiongozwa na mratibu wa utafiti kanda ilifika mkoani Njombe kwa ajili ya uchunguzi wa tatizo lililoliripotiwa.Taarifa ya awali kutoka ofisi ya mkoa ilibainisha kuwa ugonjwa ulikuwa umeathiri hadi asilimia 90 ya mavuno kwenye baadhi ya halmashauri za wilaya. Halmashauri za wilaya zilizoathirika zaidi ni pamoja na Njombe Mji, Wanging’ombe, Ludewa na Makete.

 UCHUNGUZI ULIVYOFANYIKA.

Uchunguzi ulifanyika kwa kutembelea baadhi ya mashamba yaliyoathirika, mahojiano na  maafisa kilimo mkoa, wilaya, kata na vijiji na wakulima walioathirika pamoja na uchukuaji wa sampuli za viazi na majani yenye ugonjwa kwa uchunguzi wa maabara baada ya. Jumla ya wilaya mbili (Njombe Mji na Wanging’ombe) na vijiji sita vitatu kutoka kila wilaya vilitembelewa, Kisilo, Lugenge na Matola kwa upande Njombe Mji na  Itulahumba, Igima na Ulembwe kwa upande wa Wanging’ombe.

MATOKEO YA UCHUNGUZI

3.1  Madhara ya Ugonjwa

Madhara ya ugonjwa yalikuwa makubwa kama yalivyojionyesha katika upungufu  wa mavuno uliojitokeza kwa wakulima ambapo msimu uliopita walikuwa wanavuna kati ya gunia 40 hadi 60 ukilinganisha na 2 hadi10 ya msimu huu kwa ekari ambayo ni hasara ya karibu asilimia 94%.

 

IMG_20160202_152235

Picha na.1: Moja kati ya mashamba yaliyoathirika na ukungu katika kijiji cha Utalingolo, Halmashauri ya Njombe Mji (Picha kwa hisani ya Kilumile-Afisa Kilimo).

3.2 Tatizo Halisi

Matokeo ya uchunguzi wa awali yameonyesha ugonjwa uliosababisha viazi kukauka ni ukungu unaojulikana kama ‘late blight’   ikichanganyika kidogo na ‘early blight’ kwa majina ya kitaalamu. Huu sio ugonjwa mpya bali ni ukungu uliozoeleka kwa misimu yote ambapo hushambulia viazi na nyanya lakini kwa msimu huu mlipuko wa ugonjwa uliochangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya hali ya hewa kulikosababisha kuongezeka kwa mvua na joto kama ilivyothibitishwa na wataalamu wa kilimo, wakulima karibu wote tuliowatembelea na takwimu za hali ya hewa kutoka katika kituo cha Utafiti wa Kilimo,Igeri mkoani  Njombe. Wakulima wengi walisema walikuwa wanasikia harufu kali kutoka shambani siku chache baada ya shamba kuathirika, hii ikiwa ni moja ya dalili kubwa ya shamba lililoshambuliwa na ukungu wa viazi mviringo .Sampuli za majani katika uchunguzi wa maabara pia zimeonyesha uwepo wa vimelea vya ukungu kama inavyoonekana katika picha namba 2(a&b).

 

B
 
A
 
  

Picha na. 2: Mbegu za vimelea vya ukungu  kama vinavyooonekana katika darubini (x40) A. Ukungu wa mwanzo (Early blight)  B. Ukungu wa mwisho  (Late blight)

 

Sababu  Zilizochangia Mlipuko wa Ugonjwa

Kuongezeka kwa Mvua

Ukilinganisha na misimu iliyopita (Jedwali na.1), msimu huu mvua zilikua nyingi na zilinyesha mfululizo hivyo kuvipa vimelea vya ukungu mazingira mazuri au rafiki ya kuzaliana, kukua na kusambaa. Wastani wa milimita 209.6 zilinyesha msimu huu kati ya Oktoba 2015 na Februari 2016 ukilinganisha na 166.28 za msimu wa 2014/15 na 158.12 za msimu wa 2013/14. Mbegu za ukungu husambaa kwa kuogelea hivyo uwepo wa mvua nyingi husaidia ugonjwa kusambaa kwa haraka.

 

 

 

 

Jedwali na.1: Takwimu za hali ya hewa za misimu mitatu 2013-2016 kuanzia Oktoba hadi Februari kutoka katika kituo cha hali ya hewa cha Utafiti wa kilimo Igeri, Njombe.

Msimu

Mwezi

Mvua

(Kiasi katika mm)

Mvua

(Siku)

Joto

la juu

Joto

la chini

Kiasi

cha unyevu

2013/

2014

Oct.

Nov.

Dec.

Jan.

Feb

Wastani

12.3

71.0

273.7

254.2

179.4

158.12

5

8

23

21

21

15.6

22.5

19.0

21.1

19.9

20.1

20.52

10.2

10.5

12.0

11.5

11.9

11.22

88

88

94

91

93

90.8

2014/

2015

Oct.

Nov.

Dec.

Jan.

Feb

Wastani

23.9

31.8

184.0

323.9

267.8

166.28

6

1

17

27

22

14.6

22.3

22.3

21.5

20.0

20.4

21.3

10.8

12.2

12.5

12.1

12.3

11.98

85

86

92

96

96

91.0

2015/

2016

Oct.

Nov.

Dec.

Jan.

Feb

Wastani

            8.7

           209.0

           278.2

           261.9

           290.2

209.6

2

12

19

22

17

14.4

20.7

20.5

20.4

20.5

21.8

20.78

10.1

10.4

12.1

13.0

16.5

12.42

85

88

90

97

97

91.4

 

3.3.2 Kuanza Mapema kwa Mvua

Tofauti na misimu iliyopita(Jedwali na.1), msimu huu mvuanyingi zilianza mapema hivyo ugonjwa kuanza mapema pia. Msimu uliopita na mingine ya nyuma, mvua nyingi zilikuwa zinachelewa kuanza kunyesha hivyo ugonjwa wa ukungu ukawa unachelewa kujijenga ili kushambulia viazi na ziliponyesha zilikuta viazi vimeshakomaa na hivyo kutoleta madhara makubwa. Ukiangalia jedwali na. 1, msimu huu mvua kubwa zilianza kunyesha Novemba (209mm) badala ya Desemba kama misimu mingine hivyo kupelekea ugonjwa kuanza mapema na kushambulia viazi kabla havijaanza kukomaa hivyo kusababisha madhara yaliyotokea.

3.3.3 Kuongezeka kwa joto na unyevuunyevu wa angani.

Ingawa msimu huu joto la juu halikuongezeka (Jedwali na.1), joto la chini na unyevuunyevu wa angani viliongezeka hivyo pamoja na mvua nyingi kupelekea mazingira mazuri ya kuzaliana, kukua na kusambaa haraka kwa vimelea vya ukungu. Hali ya joto la kati ya nyuzi 15 oC hadi 20 oC ndani ya siku 4 huweza kuzalisha vimelea vingi vya ukungu na kusababisha madhara makubwa. Pamoja na joto, hali ya unyevunyevu kwenye majani ya viazi ukiwa wa kuendelea zaidi ya saa 5 huleta mazingira mazuri ya vimelea vya ukungu kuzaliana kwa kasi na ndani ya muda usiopungua masaa16 hadi 24 huwa vimeshashambulia shamba lote na mkulima anapokuja kupulizia kiuatilifu hukuta vimeshajiimarisha, na ili kupambambana na kiuatilifu hutengeneza mbegu nyingi zaidi hivyo madhara kuwa makubwa zaidi mara tu baada ya kiuatilifu kupulizwa. Hali hii ndio iliyojitokeza kwa wakulima walipo jaribu kupulizia kiuatilifu mara ya pili viazi vikaungua zaidi.

3.3.4 Matumizi yasio sahihi ya viuatilifu vya ukungu na muda wa kupulizia

Wakulima wengi tuliowatembelea walitumia viuatilifu vifuatavyo vya ukungu; Rido Supa, Ivory 72, Ridomil Gold na Lincomil huku wengine wakichanganya kiuatilifu zaidi ya kimoja na kupulizia kwa pamoja. Wengi wao walikuwa wanatumia viuatilifu vya kukinga hata baada ya dalili za ugonjwa kuanza hivyo kushindwa kutibu ugonjwa na kupelekea viazi kuungua punde tu baada ya kiuatilifu kupulizwa. Mara nyingi viuatilifu vya kukinga ni bei rahisi kuliko vya kutibu hivyo wakulima kwa kujua au kutokujua hutumia viuatilifu vya kukinga.

Hata waliotumia viuatilifu vya kutibu wengine hawakufuata maelekezo ya muda wa kurudia. Muda wa kurudia hutegemea hali ya hewa hivyo kwa hali ya msimu huu ilitakiwa kurudia kila baada ya siku 7, 10 hadi 14 kulingana na nguvu ya kiuatilfu chenyewe tofauti na ilivyozoeleka ambapo kiuatilifu hurudiwa baada ya siku 14 hadi 21 kama hali ya hewa si ya mvua, joto na unyevunyevu mwingi. Ndio maana kuna wakulima mashamba yao hayakuathirika kwa sababu walitumia Ridomil kwa kiwango sahihi na kurudia kwa wakati muafaka.

Pia kulikuwa na matumizi ya kiasi kidogo cha kiuatilifu kulinganisha na dozi inayotakiwa, hii mara nyingi husababisha ugonjwa kutokingika au kutotibika. Kiasi cha vijiko vilivyokuwa vinatumika ni kati ya viwili hadi vitano kwa pampu ya lita 15. Matumizi ya kiasi kidogo cha dawa hupelekea vimelea kujenga usugu hivyo kutokingika au tibika na kiuatilifu husika.

Pamoja na kutumia kiasi kidogo cha kiuatilifu, upuliziaji pia ulionekana tatizo jingine.  Wakulima wengi, hasa wanaotumia vibarua katika zoezi la kupulizia viuatilifu shambani, mashamba yao yamekuwa yakipata kiuatifu kidogo huku mimea mingine ikikosa kabisa kutokana ulipuaji unaotokana na kasi kubwa ya kutembea inayotumiwa na wapuliziaji.

3.3.5 Matumizi ya Mbegu ya aina moja kwa muda mrefu na kwa wakulima wengi

         Wakulima wengi walioathirika wametumia mbegu aina ya CIP (KIKONDO) ambayo imetumika kwa muda mrefu sasa. Utafiti umebaini kuwa mbegu aina moja ikitumika kwa muda mrefu ni rahisi kushambuliwa na magonjwa kutokana na kupungua kwa  nguvu ya ukinzani dhidi ya vimelea vipya vinavyoweza kujitokeza. Baadhi ya wakulima waliotumia mbegu mpya kama MERU na SHEHEREKEA hawakupata madhara ya ugonjwa wa ukungu.

3.3.6 Matumizi yasiyo sahihi ya mbolea

          Mbolea zinazotumiwa na wakulima wengi ni pamoja na DAP, CAN, SA na UREA. DAP kwa ajili ya kupandia, CAN, SA na UREA kwa ajili ya kukuzia.Wakulima wengi walionekana kuchanganya mbolea zaidi ya moja bila kupata ushauri wa kitaalamu hasa ya kukuzia. Wengine walikua wanachanganya hadi na DAP ambayo ina kiasi kidogo cha naitrojeni na kiasi kikubwa cha phosphorasi ambacho hakihitajiki kipindi cha ukuaji wa viazi isipokua wakati wa kupanda. Ukiacha phosporasi ambayo haitumiki, naitrojen  ikizidi husababisha ulaini na ukuaji wa majani kupita kiasi hivyo kushambuliwa kirahisi na magonjwa.

3.3.7 Kutowatumia wataalamu wa kilimo

         Wakulima wengi walionekana kutowatumia wataalamu wa kilimo katika masuala mbalimbali yahusuyo kilimo pamoja na uwepo wao katika kila kijiji. Wengi hufanya shughuli zao kwa mazoea na kwa kubahatisha jambo linalopelekea inapotokea milipuko kama hii kupata hasara. Ili kuthibitisha hili, kuna mashamba ya baadhi ya wakulima waliofuata ushauri wa kitaalamu hayakuathirika na ugonjwa (Picha na 4). Pia mashamba darasa yaliyosimamiwa na NADO na hata ya Utafiti Igeri hayakuungua. 

 

        IMG_20160207_144850 

Picha Na.3: Mkulima katika kijiji cha Utengule, Njombe Mji akifurahia shamba alilolihudumia kwa kufuata ushauri wa kitaalamu (Picha kwa hisani ya Kilumile-Afisa Kilimo). 

4. MAPENDEKEZO

4.1 Matumizi ya utabiri wa hali ya hewa katika kilimo

Wataalamu wa kilimo wanashauriwa kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa ili kuwapa wakulima tahadhari ya uwezekano wa kutokea mlipuko wa magonjwa ya mimea na kuwashauri hatua za kuchukua.

4.2 Elimu kuhusu  matumizi sahihi ya viuatilifu na mbolea

Wakulima wengi walikiri kutokuwa na elimu ya matumizi sahihi ya viuatilifu na mbolea. Wengi wamekuwa wakitumia pembejeo hizo kwa mazoea na kubahatisha hivyo elimu ya aina gani ya kiuatilifu au mbolea itumike wakati gani kwa kiwango gani na mara ngapi kufuatana na hali ya hewa iliyopo inatakiwa kutolewa mara kwa mara kwa wakulima wetu.

4.3 Uzalishaji wa mbegu zenye ukinzani na kuzisambaza kwa wakulima.

Ili kukabiliana na milipuko ya ugonjwa wa ukungu ni vizuri kukawa na mkakati wa kuzalisha kwa wingi aina za mbegu zenye ukinzani na magonjwa zilizopo kama MERU na SHEHEREKEA na kuzisambaza kwa wakulima. Pia uwepo utafiti endelevu wa mbegu zenye ukinzani  na magonjwa. Hii itasaidia kuondoa au kupunguza athari za kukosa mavuno kabisa endapo ugonjwa utatokea.

4.4. Ushauri juu ya mbegu za viazi

       Kwa kuwa vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa ukungu hudumu muda mfupi katika udongo, viazi viliyofukiwa ndani ya udongomara nyingi  havipati mashambulizi ya ugonjwa. Hivyo Viazi vilivyovunwa kwenye mashamba yalioathirika na ukungu japo havikukomaa vinaweza kutumika kama mbegu katika msimu ujao lakini kwa tahadhari kwa kuwahi kupuliziaviuatilifu vya kutibu ukungu  kama RIDOMIL GOLD mara tu baada viazi kuota shambani. Ili kupunguza athari za kuhamisha ugonjwa kutoka msimu mmoja hadi mwingine ni vizuri kilimo cha mzunguko wa mazao (Crop rotation) kikazingatiwa.

4.5 Kufanyika kwa utafiti kubaini uwepo wa vimelea vya ugonjwa wa ukungu vilivyopo na uwezo wa viuatilifu vilivyopo kukabilina na ugonjwa wa ukungu.

Mabadiliko ya hali ya hewa mara nyingi husababisha kuibuka kwa vimelea vipya vya ugonjwa hivyo ni muhimu kufanyika utafiti kubaini vimelea vilivyopo. Hii inasaidia kuzalisha mbengu zenye nguvu kubwa ya ukinzani. Pia ni muhimu kuangalia kama viuatilifu vinavyotumika bado vina uwezo wa kukabiliana na vimelea vya ukungu au vimeshajenga usugu hivyo kuhitaji aina nyingine ya viuatilifu.

5. HITIMISHO

     Tatizo lililokumba viazi mviringo mkoani Njombe ni ugonjwa wa ukungu  unaojulikana kama ‘late blight’ ukichanganyika  kidogo na  ‘early blight’ magonjwa ambayo wakulima pia wanayafahamu na hivyo sio ugonjwa mpya. Ukungu huu ni mashuhuri kwa mashambulizi ya viazi mviringo pamoja na nyanya mahali pote mazao hayo yanapolimwa ulimwenguni, na hata katika mkoa wa Njombe wakulima wana mazoea ya kupambana nao kila msimu. Kwa msimu huu makali ya ugonjwa yamekua makubwa kupita kawaida kutokana na mabadiliko ya ghafla ya hali ya hewa hasa mvua iliyojitokeza mwezi Novemba hivyo kusababisha ugonjwa kuwahi na kuanza kushambulia viazi mapema kabla kipindi ambacho wakulima wamezoea kuanza kupiga dawa za kinga kwa tahadhari. Baada ya ugonjwa kuanza mashambani, upigaji wa dawa za kinga badala ya tiba kawaida huleta athari kwani huchochea ukungu kujenga tabia ya kuzaliana maradufu katika harakati za kukinzana na viuatilifu vinavyopulizwa, matokeo yake mazao huathirika zaidi punde tu baada ya viuatilifu hivyo kupulizwa, na hali hii ndiyo iliyojitokeza katika mashamba ya wakulima. Katika hali hii wakulima walitakiwa kupiga dawa ya tiba badala ya kinga.

      Elimu ya matumizi sahihi ya viuatilifu, mbolea, utabiri wa hali ya hewa, mbegu bora zenye ukinzani pamoja na ushauri wa wataalamu wa kilimo vitasaidia kudhibiti hali kama hii isijitokeze tena wakati ujao.  Pia utafiti zaidi  wa tathmini ya aina ya vimelea vya ukungu vilivyopo  katika mazingira ya Tanzania unatakiwa kwani utasaidia kubaini  uzukaji wa    vimelea vipya vinavyoweza kusababisha  madhara makubwa hata zaidi mfano wa njaa kubwa ya kihistoria iliyotokea huko Ireland miaka ya nyuma. Vilevile utasaidia kuzalisha aina bora za mbegu za viazi zenye ukinzani mpana.

      Kutokana na madhara ya ugonjwa wa ukungu kuna upungufu mkubwa viazi na mbegu. Hivyo Viazi vilivyovunwa kwenye mashamba yalioathirika na ukungu japo havikukomaa vinaweza kutumika kama mbegu katika msimu ujao lakini kwa tahadhari kwa kuwahi kupuliziaviuatilifu vya kutibu ukungu  kama RIDOMIL GOLD mara tu baada viazi kuota shambani  Kwa kuwa vimelea vinavyosababisha ugonjwa wa ukungu hudumu muda mfupi katika udongo, viazi viliyofukiwa ndani ya udongo mara nyingi  havipati mashambulizi ya ugonjwa

 


Viewing all articles
Browse latest Browse all 2276

Trending Articles