Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma,
SACP David Misime
Napenda kutoa taarifa fupi kuhusu tukio lililotokea tarehe 11/07/2015 majira ya saa
10:00 hrs huko katika Hoteli ya St. Gasper hapa mjini Dodoma, kuwa wananchi
walitoa taarifa majira ya saa nne asubuhi kwamba kuna mtu mmoja mwenye asili ya
Kiasia amekamatwa na wananchi akiwa na fedha nyingi na kuna vurugu kubwa.
Baada ya kupata taarifa hizo Jeshi la Polisi Mkoani hapa lilifika eneo la tukio ili
kuona kama taarifa hizo ni za kweli.
Askari walithibitisha kuwa ni kweli walimkuta mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia ambaye alijulikana kwa jina la AMIT KEVALRAMANI mwenye umri wa miaka 31, Mhindi, Mfanyabiashara, Mkazi wa
Dar es Salaam akiwa na fedha kiasi cha Tshs. 722,500,000/=
ambacho alipohojiwa alisema kuwa tarehe 10/07/2015 alifika Dodoma kwa ajili ya
ununuzi wa mazao ya nafaka.
Alipofika Dodoma tarehe 10/07/2015 majira ya
asubuhi alifikia katika Hoteli ya St. Gasper na tarehe 11/07/2015 aliamua
kurudisha fedha benki kutokana na kuona mkusanyiko wa watu wengi wasioeleweka
na wenye viashiria vya vurugu.
Akiwa katika harakati ya
kurejesha fedha hizo benki, ndipo kundi la watu waliokuwa katika eneo la Hoteli
ya St. GASPER walimtilia mashaka na kumzuia asiondoke na ndipo taarifa
zilitolewa polisi. Mashaka ya watu hao yalitokana na vuguvugu za
kisiasa/mchakato wa uchaguzi kati ya makundi mbalimbali kuwa kuna watu
wanahonga wajumbe. Taarifa za aina hiyo ambazo hata Jeshi la Polisi lilikuwa
limepokea bila uthibitisho.
Katika tukio hili na
uchunguzi tulioufanya tumebaini kuwa hakuna kosa la jinai lililothibitika licha
ya kukutwa na kiasi hicho cha fedha, tuhuma za rushwa ambazo ndiyo zilikuwa
msingi wa ukamataji wa mtu huyo hazikuthibitika, kwa kuwa hakuna aliyeona
akizigawa fedha hizo wala hakuna aliyedai kushawishiwa au kugawiwa fedha hizo.
Aidha imethibitika fedha
hizo ni mali yake halali na kwa kuwa hakuna ushahidi mwingine uliyo thibitisha
vinginevyo amerejeshewa fedha zake.