Trump aahidi umoja na mabadiliko kabla ya kuapishwa Marekani![Trump na Mike Pence wakiweka shada la maua makaburi ya taifa ya Arlington]()

Akiongea katika vidato vya sanamu ya ukumbusho wa Lincoln mjini Washington DC, rais huyo mteule pia aliahidi kuleta mabadiliko.
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo iliyodumu saa mbili ni mke na watoto wake, mwigizaji Jon Voight na mwanamuziki aliyeimba wimbo wa Soul Man, Sam Moore.
Bw Trump baadaye aliweka shada la maua katika makaburi ya taifa ya Arlington, Virginia.
Hafla hiyo ya Make America Great Again! (Fanya Marekani kuwa kuu tena) ilikuwa wazi kwa umma kuhudhuria na miongoni mwa waliotumbuiza ni nyota wa muziki wa country Toby Keith na
Lee Greenwood.
"Tutaunganisha nchi yetu," Bw Trump alisema mwishoni mwa tamasha hilo.
"Tutaifanya Amerika kuwa taifa kuu tena kwa ajili ya watu wetu wote. Kila mtu, kila mtu, kote nchini. Na hii inajumuisha hata walio mitaa duni."
Wafuasi wake wamekuwa wakitiririka kuingia Washington DC, na aliwakumbusha kwamba kuna watu wengi ambao walidhani hangeshinda urais.
"Walisahau kuhusu wengi wetu,"alisema.
"Kwenye kampeni, niliwaita mwanamume aliyesahaulika na mwanamke aliyesahaulika. Naam, sasa nyinyi si watu waliosahaulika tena."
"Mambo yatabadilika, nawaahidi. Mambo yatabadilika."
Alisema atafanya mambo ambayo hayajafanywa nchini Marekani mwa miongo mingi.
Mkewe Melania aliambia waliohudhuria tamasha hilo kuwa: "Kesho tunaanza kazi."