ANAONEKANA mbele ya macho ya baadhi ya wanasiasa ndani ya chama chake kama mwanachama mkorofi. Anachukiwa na wengine kwa sababu ya kutochunga ulimi wake.
Lakini pia mwanasiasa huyu kijana anachukiwa na kundi la mafisadi ndani ya chama chake kwa sababu mara kadhaa ametoa kauli zilizowachoma na kuwaumbua vibaya watawala na watendaji wa serikali wanaotumia vibaya madaraka yao kupoka na kupora haki za wanyonge.
Huyu ni Deo Filikunjombe, Mbunge wa Ludewa (CCM), ambaye ni mmoja wa wabunge wa chama hicho tawala, ambaye maneno, matendo na misimamo yake imekuwa ikikinzana na wengi ndani ya chama hicho kiasi cha kumletea maadui wengi.
Filikunjombe ambaye ni mmoja wa wabunge vijana, amekuwa ‘mwiba’ mkali hata kwa watendaji wakuu wa serikali.
Hili lilijidhihirisha alipokuwa mmoja wa wabunge kutoka ndani ya CCM walioweka saini zao kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Hatafuni maneno, wala hatoi mawazo yake kwa sauti ya nguvu, kali wala kufoka.
Anaposimama kuchangia hoja bungeni, kwa mtu asiyemjua vema ama aliyemwona kwa mara ya kwanza, atadhani mbunge huyu hana ama hajui kile anachotaka kukisema.
Hutoa hoja yake kwa sauti ya upole, lakini iliyojaa maneno makali, magumu, mazito na yaliyomeza uzito wa ukweli. Ni mbunge ambaye huchangia hoja kwa kutazama mwelekeo na hadhi ya nchi.
Ni mbunge anayeangalia kwanza hatima ya taifa lake, kisha chama chake baadaye. Kwa msimamo huo, huzungumza kile ambacho asilimia kubwa ya wabunge wenzake ndani ya CCM hukiamini kuwa si chake bali kilicholishwa kinywani mwake na watu wa kambi ya upinzani.
Dhana hii inakuja kutokana na namna alivyo rafiki mkubwa na wabunge wengine wa upinzani, lakini kubwa zaidi akiaminiwa kuwa mwenendo, lugha na matamshi yake; kwa matarajio ya wanasiasa wengi ndani ya CCM ni kariba ya wapinzani.
Wakati ndani ya CCM akionekana ‘mkorofi’ akiwa ameitwa mara kadhaa kuonywa, nje ya chama chake hususan jimboni kwake ni lulu.
Wakati baadhi ya wabunge wakiogopa kurejea katika majimbo yao, ama wakichagua maeneo ya kutembelea majimboni, hali ni kinyume kwa Filikunjombe.
Wakati baadhi ya wabunge wakionekana kuwa mzigo na wakati mwingine kulazimika kutoa rushwa ya vyakula ama vitu vya ovyo, ili kutafuta uhalali katika majimbo yao, kwa Filikunjombe ni tofauti kama anavyosema mmoja wa wakazi wa Jimbo la Ludewa.
“Ndugu Katibu Mkuu, ninapenda kukwambia wazi kwa kipindi kirefu tangu uhuru wa nchi yetu hatujawahi kupata mbunge wa aina yake kama huyo ambaye amekuwa akipigania maendeleo ya jimbo letu na wilaya hii ya Ludewa.
Hapa Mlangali kila mwananchi anaona heshima ya wilaya hii isingekuwa hivi ilivyo bila uongozi wa miaka miwili ya ubunge wa Filikunjombe,” anasema mwananchi huyo aliyetambuliwa kwa jina la Neema Mwinuka.
Kauli hii ilitolewa wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, katika Jimbo la Ludewa hivi karibuni.
Ilikuwa ni ziara ya siku mbili ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, ambaye aliongozana na Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa CCM taifa, Nape Nnauye, waliokuwa wakikagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.
Akiwa ameshangazwa na mapokezi ya wananchi, baadhi yao wakionekana wazi kuwa wanachama wa vyama vingine vya upinzani, kinyume kabisa na kote walikotangulia, Kinana na viongozi wenzake walishangazwa kupokewa na mabango yaliyoandikwa: ‘Jembe, Jembe, Jembe’
“Jembe ndiyo nini?” Kinana alisikika akiuliza; kisha kujibiwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, Deo Sanga:
“Hapa kwetu, Jembe ni Mheshimiwa Deo Filikunjombe.
Wananchi wamempa jina hili kutokana na kuridhishwa kwake na kazi za maendeleo anazozifanya katika jimbo hili na ndiyo maana wakamlinganisha na jembe.”
Haikushangaza basi kwa Kinana kumkabidhi rungu Mbunge Filikunjombe, akimtaka alitumie kama silaha ya kuwatumikia wananchi kwa kasi zaidi, kwa kile alichosema kuwa “kuridhika kuwa kipenzi cha wananchi.”
Wahenga walisema ukitaka cha uvunguni sharti uiname. Ndivyo ilivyotokea kwa mbunge huyu. Pamoja na kuwapo kwa watu wanaopinga juhudi zake na wengine kufikia hatua ya kumshambulia kwa makosa ya hapa na pale ambayo Katibu Mkuu Kinana aliyaita majungu, ukweli unabaki kuwa, amefanya mengi katika Jimbo la Ludewa ambalo kwa miaka mingi limekabiliwa na matatizo mengi ya kimaendeleo.
Ushahidi wa haya ni kauli za wananchi wenyewe, mbele ya Kinana. “Mheshimiwa tunaomba sana leo muone namna tunavyopata tabu kutokana na barabara zetu.
Hizi unazoziona zikiwa katika hali ya unafuu zinatokana na juhudi binafsi za mbunge huyu.
“Mbunge wetu amekuwa akipigania maendeleo ya jimbo hili ambalo halina barabara na baadhi ya maeneo yalikosa kabisa mawasiliano ya simu. Lakini sasa mambo yamekwenda sawia,” alisema mwananchi mwingine, Patrick Joseph.
Zipo kauli zilizosukuma lawama moja kwa moja kwa uongozi wa juu wa CCM kwa kumshambulia na kumwona mbunge huyu kama mkorofi.
Wananchi wakaitaka CCM kuacha mchezo huo wa kusakama wawakilishi wa wananchi wanaosimamia ukweli na maendeleo ya wale waliowachagua.
Kauli hizi na nyingine zilizoonekana kumchoma Kinana na ujumbe wake, zikamfanya mtendaji huyo mkuu wa chama tawala kuahidi kuwa hakuna mtu atakayemsakama tena mbunge wao, Filikunjombe!
Kinana akaenda mbali zaidi akiwataka wabunge wa CCM kuiga mfano wa Filikunjombe kwa kuwasemea wananchi waliowachagua na kuwa mbunge wa watu, hata kama watachukiwa kwa ukweli wao.
“Mimi si Mwana CCM bali ninamkubali sana Filikunjombe kutokana na utendaji wake ndani ya Bunge na nje, ambao ni wazi umekuwa na neema na heshima kwetu Wana Ludewa,”
alisema mmoja wa wananchi aliyetambuliwa kwa jina moja tu la Haule mbele ya Kinana, huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliofika katika mkutano wa hadhara.
Je, kauli ya Kinana itapewa uzito kwa kiasi gani? Je, Deo Filikunjombe, mwanasiasa kijana na mwandishi wa habari kitaaluma hatasakamwa tena kwa ukweli wake na kusimamia masilahi ya taifa bila ubaguzi?
KWA hisani ya fg blog