MKUU WA WILAYA YA NJOMBE BI.SARAH DUMBA AWATAKA WANANCHI KUCHANGIA MCHANGO WA UZOAJI TAKA Tshs 3000/=
Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Sarah Dumba amezikumbusha halmashauri za mji wa Njombe na Makambako kuhakikisha zinatekeleza jukumu la kuondoa taka kwenye vizimba vya taka hizo ambapo pamoja na mambo mengine wananchi nao wameombwa kushiriki uchangiaji fedha kwaajili ya kusaidia kuondoa uchafu huo.
Akizungumza na mtandao huu Mkuu wa Wilaya ya Njombe bi.Sarah Dumba amesema kuwa ili halmashauri iweze kupatiwa hati safi ya usafi wa mazingira wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa na vijiji wanatakiwa kutambua umuhimu wa
kuchangia kuliko kuiachia halmashauri pekee jambo ambalo hazitaweza kumudu uzoaji wa taka hizo.
Aidha Bi.Dumba amesema kuwa kutokana na ongezeko la wakazi wa halmashauri za mji wa Njombe na Makambako uzalishaji wa taka umekuwa ukiongezeka siku hadi siku tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo jitihada mbalimbali zinatakiwa kufanyika katika kuhakikisha usafi wa mazingira unakuwepo ili kuepukana na milipuko ya magonjwa.
Kauli hiyo ya Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi.Dumba imekuja kufuatia kuwepo kwa takataka nyingi kwenye vizimba mbalimbali Mjini Njombe na Makambako jambo linalotishia usalama wa afya za wakazi wa maeneo hayo ambapo amesema cha kushangaza zaidi baadhi ya wananchi wanatupa uchafu huo kwenye vyanzo vya maji.
Halmashauri za mji wa Njombe na makambako tayari zimekwisha kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo hilo ambapo kwa halmashauri ya mji wa Makambako imekwisha pata gari la kuzolea taka hizo huku halmashauri ya mji wa Njombe ikiwa na magari mawili kwaajili ya kuzolea taka hizo na kuweka miji katika hali ya usafi.
kwa hisani ya matukio na ngilangwa